Bei mpya za mafuta kuanzia leo baadhi ya Mikoa

Jumatano , 6th Feb , 2019

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza bei mpya za mafuta ambazo zimepungua ikilinganishwa na mwezi uliopita.

Picha ya gari likijaza mafuta Sheli.

Taarifa iliyotolewa na kaimu mkurugenzi wa Ewura, Nzinyangwa Mchany inasema bei hizo mpya zitaanza kutumika kuanzia leo Jumatano Februari 6, 2019.

Inaeleza kuwa bei za jumla na rejareja kwa mafuta yaliyoingizwa nchini Tanzania kupitia Bandari ya Dar es Salaam, zimepungua kwa viwango tofauti. Inaonyesha kuwa wateja wa rejareja watapata unafuu wa shilingi 175 kwa lita ya petroli wakati wale wa dizeli wakishushiwa kwa shilingi 144 na mafuta ya taa shilingi 156.

Hata kwa bei za jumla, petroli imepungua kwa shilingi 174.03 kwa lita, dizeli kwa shilingi 143.65 na mafuta ya taa shilingi 155.32 na kueleza kuwa kupungua kwa bei hizo kunatokana na kuendelea kushuka kwa bei katika soko la dunia.

Licha ya mabadiliko hayo ya bei, mikoa ya kaskazini itabaki kama mwezi uliopita kutokana na kuwapo kwa shehena iliyopokelewa Januari, 2019 kupitia Bandari ya Tanga huku kukiwa bado kuna akiba kubwa iliyoingizwa Desemba 2018.

Inafafanua kuwa bei za mafuta kwa mikoa ya kusini zilikokotolewa kulingana na gharama za mafuta yaliyopokelewa katika Bandari ya Dar es salaam lakini wiki ya pili ya Januari Bandari ya Mtwara ilipokea shehena ya petroli hivyo kubadili ukokotozi.

Kuanzia Januari 25, 2019 bei ya rejareja ya petroli na dizeli katika mikoa hiyo zilikokotolewa kwa gharama za Bandari ya Mtwara hivyo zitaendelea kubaki kama zilizvyo kuanzia tarehe hiyo.