Jumanne , 29th Jul , 2025

ACTIF ilianzishwa mwaka 2022 kwa lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kiutamaduni baina ya mataifa ya Afrika na Karibiani.

Jukwaa la Nne la Biashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (ACTIF) limetakiwa kuja na majibu ya changamoto za kibiashara na uwekezaji zinazoyakabili mataifa ya Afrika na yale ya eneo la Karibiani.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  jana Jumatatu, Julai 28, 2025 wakati akishiriki mjadala ya Wakuu wa Nchi na Serikali kwenye ufunguzi wa jukwaa hilo linalofanyika katika kituo cha mikutano cha Radisson jijini St. George’s, nchini Grenada.

 Waziri Majaliwa amesema kuna haja ya kutengeneza mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye mataifa wanachama akitoa mfano wa Tanzania, ambapo Aliko Dangote amewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye ujenzi wa kiwanda cha saruji.

Viongozi wengine walioshiriki mjadala huo ni Waziri Mkuu wa Dominica, Roosevelt Skerritt; Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Amor Mottley; Waziri Mkuu wa Antigua and Barbuda, Gaston A. Browne; Waziri Mkuu wa Saint Kitts and Nevis, Dkt. Terrance Drew; Waziri Mkuu wa St. Lucia, Philip J. Pierre pamoja na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Prudence Sebahizi.

Katika kipindi cha miaka mitatu, jukwaa hilo limewezesha kuimarika kwa ushirikiano baina ya sekta za umma na binafsi, kusainiwa kwa hati za makubaliano na ushirikiano zenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni nne; hatua ambayo imechochea wazo la kuanzisha ukanda rasmi wa biashara kati ya nchi za Afrika na Karibiani.