Panya asababisha hasara ya dola milioni 190

Alhamisi , 13th Sep , 2018

Migahawa maarufu nchini China imepoteza kiasi cha Dola milioni 190 katika thamani ya soko baada ya mama mmoja mjamzito kukuta panya aliyekufa kwenye supu kwenye moja ya migahawa hiyo.

Pichani mnyama Panya.

Hisa za migahawa hiyo ya Hotpot imeporomoka vibaya, baada ya picha za panya huyo aliyekufa akitolewa kwenye bakuli la supu kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo mgahawa wake katika Jimbo la Shandong, umefungwa kwa muda.

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa Kankan News, mgahawa huo ulimpa mama huyo Dola za Kimarekani 729 kama fidia kufuatia tukio hilo, lakini alizikataa.

Mwanamke huyo mjamzito ambaye alikwenda katika mgahwa huo pamoja na familia yake mnamo Septemba 6 alimuona panya aliyekufa wakati tayari akiwa amekula vipande kadhaa vya nyama kwenye supu.

Taarifa zaidi zinasema mmoja wa wafanyakazi wa mgahawa huo alimshauri mume wa mama mjamzito atoe mimba kama ana wasiwasi kuhusu afya ya kichanga chake na kuahidi kumpa fedha kwa ajili ya kuavya mimba yake.