Alhamisi , 28th Jan , 2021

Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda, amesema kwamba Tanzania bado inauhitaji wa kuagiza sukari kutoka nje ya nchi kiasi cha Tani 40 kwa kuwa bado viwanda vya ndani havijitoshelezi katika uzalishaji wake.

Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda

Profesa Mkenda, ameyasema hayo Jijini Dodoma, baada ya kukutana na Bodi ya Sukari nchini ambapo amesema Tanzania kwa sasa inazalisha Tani 377,000, ambapo wakulima wamelima miwa mingi lakini tatizo lipo kwenye uchakataji wake kwa kuwa viwanda haviwezi kuchakata miwa yote inayolimwa.

"Bado kuna uwezo wa kuzalisha sukari ya kutosha nchini kwa kuwekeza tu na kuhakikisha kwamba uwezo wa kuchakata miwa yote inayolimwa unaongezeka hivyo miwa haibaki shambani na kuongeza tija kwa aina bora ya mbegu na miundombinu ya umwagiliaji ni hivyo tu tutafikia mahitaji yetu yote ya sukari tunayoyahitaji", amesema Profesa Mkenda.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Sukari Tanzania, Mwamini Malema, ameyataka makampuni ya sukari kuhakikisha yanazalisha kwa tija na kwa ushindani ili kuongeza soko kimataifa na kuzuia uhaba wa sukari kwa siku za mbeleni.