Jumatatu , 19th Oct , 2020

Tarehe 12 Oktoba ukanda wa Afrika Mashariki ulishuhudia nchi ya Rwanda, kupitia Bodi ya Maendeleo ya Taifa hilo (Rwanda Development Board) ikiidhinisha na kupitisha kilimo cha bangi nchini humo ambapo bangi itakayozalishwa nchini humo, itatumika kimatibabu na kuuzwa kwa makampuni ya kigeni

Picha ya zao la mmea wa bangi

Ukanda wa Afrika Mashariki unafikisha nchi mbili ambazo sheria zake, zinaruhusu kilimo cha bangi ambapo nchi ya Uganda ilifanya hivyo mwaka 2019. 

Kwa nchi za Afrika Lesotho, ndiyo lilikuwa taifa la kwanza kuidhinisha kilimo cha bangi kisheria mwaka 2017 ikifwatiwa na Zambia mwaka 2019 huku Afrika Kusini mwaka 2018 ikihalalisha matumizi ya bangi ili kujistarehesha.

'' Sekta rasmi ya kilimo cha bangi barani Afrika itafikia hadi dola bilioni 7.1 kwa mwaka ifikapo  2023 kama uhalalishwaji utafanyika katika masoko makubwa ya Bara la Afrika'' hii ni kwa mujibu wa The African Cannabis Report.

Ikiwa inatizamwa kama fursa kwa mamilioni ya wakazi wa Afrika, sheria na taratibu kadhaa nazo zimewekwa na mataifa hayo katika kilimo cha bangi. 

Mfano kwa Zimbabwe Wizara ya Afya ya taifa hilo inahusika na utoaji wa vibali na leseni kwa makampuni na watu binafsi ambao wamekidhi vigezo vya kulima kilimo cha bangi kwa kibali cha miaka mitano.

Mwezi Februari mwaka 2020 imekuwa zamu ya nchi ya Malawi huku mataifa mengi mengine barani Afrika yakiwamo Tanzania na Kenya yakiwa yamewahi kujadili masuala yanayohusiana na kilimo na biashara ya bangi katika majengo ya Bunge, jambo ambalo linashiria kuwa katika siku za usoni huenda mataifa mengi ya Kiafrika yakafuata mkondo wa Rwanda na nchi zingine.