
Jeshi la Polisi limethibitisha kuwakamata watu 12 ambao ni waendesha pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda katika Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya mkoani Mara baada ya kufanya fujo na kufunga barabara katika mji wa Sirari jana Oktoba 21, 2025.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi katika Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya imesema kuwa chanzo cha fujo hicho kimetokana na kukamatwa kwa vijana wawili (2) mnamo majira ya saa 11: 30 jioni kwa mujibu wa sheria na kuwafikisha katika Kituo cha Polisi Tarime.
“Baada ya watuhumiwa hao kufikishwa kituoni, vijana wa bodaboda waliopewa taarifa potofu na ambao walishuhudia watuhumiwa hao kufikishwa kituoni walirudi eneo la mji wa Sirari na bila halali yoyote na kwa makusudi wakajaribu kufanya fujo na kufunga barabara,” taarifa hiyo imesema.
Jeshi la polisi liliwatawanya vijana hao na kufanikiwa kuwatia nguvuni bvijana hao 12 na watachukuliwa hatua pindi taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la polisi Tarime Rorya limewataka wenye tabia za kufanya fujo kuacha mara moja kwani watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.