Jumatano , 12th Nov , 2025

Watu 38 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za kuingia nchini kinyume cha sheria.

Watu 38, akiwemo raia mmoja wa Ethiopia, Tadesa Limoli (32), wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za kuingia nchini kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga amethibitisha katika taarifa kuwa, watuhumiwa hao walikamatwa Novemba 11, 2025, katika Pori la Ranchi ya Matebeteli, Wilaya ya Mbarali, mkoani humo walipokuwa wakisafiri kwa gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T.953 DJF, mali ya Stanslaus Mazengo, mkazi wa Isitu, ambaye ndiye alikuwa dereva wa gari hilo.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Mazengo alikuwa akiwapeleka wahamiaji hao katika nyumba ya Jackline Malya (26), mkazi wa Chimala, kwa lengo la kuwahifadhi kabla ya safari ya kuwavusha kwenda Afrika Kusini kwa njia zisizo rasmi,” amesema Kamanda Kuzaga.

Aidha, Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa wananchi kuacha tamaa ya fedha inayowasukuma kushiriki vitendo vya kuwawezesha raia wa kigeni kuingia au kupita nchini bila kufuata taratibu za kisheria, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo.