Jumamosi , 10th Jan , 2015

Utafiti unaonesha kuwa 50% ya akina mama wajawazito mkoani Shinyanga, hujifungulia kwa wakunga wa jadi, hali ambayo imekuwa ikichangia kuongezeka kwa idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Ntuli Kapologwe

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Ntuli Kapologwe, amesema baadhi ya wajawazito mkoani humo hawahudhurii kwenye vituo vya afya na kliniki na kusababisha wanawake 64 kupoteza maisha katika kipindi cha mwaka 2014 kutokana na kujifungulia nyumbani na kukosa huduma muhimu pale walipopata matatizo wakati wa kujifungua.

Amesema vifo vingi kwa akina mama hao vinachangiwa na mila na desturi na kuwa wanawake wanao pata ujauzito wakiwa na umri mkubwa wamekuwa wakiona aibu kwenda vituo vya afya na kwenye hospitali kuzalishwa na wauguzi wenye umri mdogo.

Dkt. Kapologwe amesema kutokana na hali hiyo tayari wameanza kutoa elimu kwa akina mama hao, kujua umuhimu wa kujifungulia hospitalini, zahanati au vituo vya afya huku akiwataka kuwaamini wauguzi wenye umri mdogo kuwa kazi wanayoifanya ni ya kitaaluma.