Jumatatu , 13th Apr , 2015

Chama cha ACT Tanzania kimemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Jakaya Kikwete kuitisha bunge ili kufanyia marekebisho katika baadhi ya vifungu kwenye Katiba ya mwaka 1977 kwa lengo la kuingiza baadhi ya mambo ikiwa ni pamoja na kuunda tume huru.

Kiongozi mkuu wa chama cha ACT, Zitto Zuberi Kabwe akiwahutubia wananchi wa Njombe.

Mwenyekiti wa chama hicho Bi. Anna Mghwira amesema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara mjini Njombe na kueleza kuwa marekebisho hayo yataondoa malalamiko ya baadhi ya vyama hasa vya upinzani juu ya uwepo wa hujuma katika zoezi zima la uchaguzi mkuu pamoja na chaguzi ndogo zitakazofuata.

Kwa upande wake kiongozi wa chama hicho Bw. Zitto Kabwe amesema chama chake kimeamua kuelekeza nguvu katika kupambana kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika ipasavyo na kumfaidisha kila mwananchi badala ya wageni na watu wachache kujinufaisha binafsi.

Viongozi wa chama cha ACT-Tanzania wapo katika ziara ndefu wakipita mikoa mbalimbali na kufanya mikutano ya hadhara kwa lengo la kukitambulisha chama hicho kipya kwa wananchi huku kikitafuta uungwaji mkono katika medani ya siasa za ushindani.