Alhamisi , 7th Nov , 2019

Chama cha ACT-Wazalendo, kimemuomba Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo, asimamie mwenyewe zoezi la kurejeshwa kwa majina ya wagombea, walioenguliwa katika zoezi la uteuzi wa wagombea wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kinyume cha taratibu ili kuhakikisha haki inatendeka.

Katibu Mkuu ACT - Wazalendo Dorothy Semu

Rai hiyo imetolewa leo Novemba 7, 2019, na Katibu Mkuu wa chama hicho Dorothy Semu, ambapo pia chama hicho kimetoa maelekezo kwa wagombea wao nchi nzima, kuhakikisha wanazifuatilia rufaa dhidi ya kutenguliwa kwao kwenye mamlaka husika.

"Tunaiomba TAMISEMI kusimamia kurejeshwa kwa wagombea wetu nchi nzima ambao wameenguliwa majina yao  bila sababu yoyote ya msingi, chama pia kimefanya mawasiliano na vyama vingine vya upinzani ili kuunganisha nguvu ya kukabiliana na hujuma zilizofanyika" amesema Dorothy Semu.

Novemba 5, 2019, Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo, aliziagiza kamati za rufaa kusikiliza vyema kero za watu wenye malalamiko, ikiweno za wagombea waliokatwa majina yao na kuhakikisha wanayarejesha ili na wao waweze kupata haki zao za msingi.