Alhamisi , 19th Sep , 2019

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya imemuhukumu kunyogwa mpaka kufa kijana Amani Kalinga (21), Mkazi wa Kijiji cha Mpanda Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, baada ya kukutwa na hatia kwa kosa la kuuwa kwa kukusudia.

Akitoa hukumu hiyo Jaji wa Mahakama Kuu, Dk. Adam Mambi amesema kutokana na kosa la mtuhumiwa huyo kuua kwa kukusudia na kuchukua viungo vya sehemu za siri za mtoto Heroni Kalinga (12), ameeleza adhabu hiyo ni fundisho kwa vijana wengine wanaoamini imani za kishirikina.

Akisoma shauri hilo mahakamani, Wakili wa serikali, Shindani Michael amesema kuwa mshitakiwa alifanya kosa hilo mwaka 2017 nyumbani kwao Kijiji cha Mpanda,  ambako aliwakuta watoto zaidi ya watano wakichunga Ng’ombe na ndipo alipomshika marehemu na kumchoma kisu, na kuchukua sehemu zake za siri.

Hata hivyo Wakili wa Serikali, ameishukuru Mahakama kwa kutoa hukumu hiyo ambayo ameomba iwe fundisho kwa wananchi wanaoaamini imani za kishirikina.