Agnes James (36) amefariki dunia huku wengine saba wakinusurika kifo kufuatia ajali ya moto, iliyotokea katika nyumba waliyokuwa wanaishi katika Mtaa wa Mwasele “B”, Kata ya Kambarage, Manispaa ya Shinyanga.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, limesema chanzo cha moto huo ni shoti ya umeme iliyosababishwa na matumizi ya vyombo vingi vya umeme kwa wakati mmoja kwenye soketi za umeme huku likiwatahadharisha wananchi kuzingatia usalama wa vyombo vya moto majumbani.
Kwa upande wao, mashuhuda wa tukio hilo wamesema moto huo ulianza ghafla na kusambaa kwa kasi hali iliyowafanya kushindwa kuokoa mali wala kuingia ndani ya nyumba.
Balozi wa Nyumba Kumi Bi. Rehema Shimiu pamoja na Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwasele “B”, Bw. Cosmas Lucas, wamesema juhudi za pamoja na Jeshi la Zimamoto, hazikufanikiwa kuokoa maisha ya mama huyo kwa kuwa moto ulikuwa mkubwa uliokuwa unateketeza mali zilizokuwa ndani ya nyumba hiyo.

