Jumatano , 22nd Jun , 2016

Serikali imesema juhudi za ujenzi wa uchumi wa viwanda zimeanza kuonekana kupitia ongezeko maombi ya wafanyabiashara wanaotaka kufungua viwanda maeneo mbali mbali nchini, sekta ambayo ndiyo tegemeo la kuongeza fursa za ajira na kukuza pato la taifa.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji mhandisi Joseph Malongo

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji mhandisi Joseph Malongo amesema hayo leo wakati wa utoaji wa ruzuku kwa kampuni tano za wajasiriamali wazawa, walioamua kuwekeza kwenye mnyororo thamani wa mazao ya kilimo, ruzuku iliyotolewa na Mfuko wa Kichocheo unaosimamiwa na Ukanda wa Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania – SAGCOT.

Kauli ya mhandisi Malongo imetokana na swali la wanahabari waliotaka kufahamu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa dhana ya uanzishaji wa viwanda kama mkakati wa kufikia dira ya maendeleo ya inayolenga kuiwezesha Tanzania kuwa taifa la uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Kumekuwa na maswali kwamba hii dhana ya viwanda je inatekelezea? Ukweli ni kwamba juhudi za kuanzisha viwanda zimeanza kuonekana kwani tayari viwanda vimeanza kujengwa maeneo mbali mbali nchini na hata idadi ya wafanyabiashara wanoomba kuanzisha viwanda vipya nayo imeongezeka,” amesema mhandisi Malongo.

Amesema kamwe serikali haitahusika na ujenzi wa viwanda hivyo isipokuwa vile tu vya kimkakati na kwamba katika kutekeleza hilo jukumu la serikali ni kuandaa mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuweza kuanzisha viwanda na kufikia masoko ya bidhaa zitakazozalishwa katika viwanda hivyo.

Amesema hata utoaji wa ruzuku kwa kampuni za wajasiriamali wazawa ni baadhi tu ya mipango iliyopata baraka na usaidizi wa serikali kwa kuhakikisha wajasiriamali hao wanaongeza na kuboresha uzalishaji kupitia uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vitakavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo.

“Ukiangalia kati ya waliopata ruzuku leo wapo wanaozalisha moja kwa moja, wapo wanaowawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na wapo wanaongeza thamani bidha na mazao kutoka

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa SAGCOT Bw. John Kyaruzi ametaja sababu za kutolewa ruzuku hiyo kuwa ni haja ya wadau wa kilimo nchni ya kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo na kubadili hali ya kiuchumi ya wakulima na wafugaji.

Amesema kuwa hata mipango ya kuipeleka Tanzania kuwa taifa la uchumi wa kati inategemea sana ujenzi wa viwanda ambavyo malighafi zake zitatokana na kilimo sambamba na viwanda vyenyewe kutengeneza sana bidhaa za kilimo.