Mfanyabiashara Mtanzania, Rostam Azizi rasmi sasa anakuwa mbia mkuu wa kampuni ya habari ya Nation Media Group (NMG) baada ya kampuni ya Aga Khan Fund for Economic Development (AKFED) kutangaza kuuza hisa zake zote zilizokuwa zikimilikiwa katika kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumanne, Machi 10, 2026, AKFED imeingia makubaliano ya kuuza umiliki wake wa asilimia 100 katika kampuni ya NPRT Holdings Africa Limited kwa kampuni ya Taarifa Ltd inayomilikiwa na Rostam Azizi.
Nation Media Group ni moja ya kampuni kubwa za habari Afrika Mashariki ikiwa na shughuli katika nchi za Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda. Kampuni hiyo inachapisha magazeti mbalimbali yakiwemo Daily Nation, Sunday Nation, The EastAfrican, Daily Monitor ya Uganda pamoja na Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti nchini Tanzania. Pia inamiliki Televisheni ya NTV Kenya na Uganda na vituo vya redio Kenya, Uganda na Rwanda.





