Ajira za upendeleo kwa vijana Bomba la Hoima

Jumatatu , 12th Apr , 2021

Mbunge wa Kiteto Mhe. Edward Kisau Olelekaita, amehoji juu ya suala la uwepo wa ajira za upendeleo pamoja na fursa nyingine kwenye ujenzi wa bomba la mafuta la Hoima - Tanga kutokana na mradi huo kupita kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwemo wilaya ya Kiteto.

Sehemu ya bomba la mafuta la Hoima - Tanga

Mbunge Olelekaita amehoji hilo leo Aprili 12, 2021, bungeni kwenye kikao cha 7, mkutano wa 3 wa bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akijibu swali hilo Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema vijana wanayo nafasi ya kupata ajira kwenye ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Uganda.

''Mheshimiwa Spika, kutokana na Bomba hilo kupita katika Wilaya ya Kiteto, wananchi wa Kiteto wanufaika na ujenzi wa mradi huo kwa kufanya biashara, ajira na fursa za kiuchumi na kijamii. Utekelezaji wa kazi za mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Julai, 2021 na kukamilika mwezi Julai, 2023,'' amesema Waziri Dkt. Kalemani.

Aidha, Dkt. Kalemani ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wadau wengine, inaendelea kutoa hamasa ili wananchi wanufaike na shughuli za ujenzi na uendeshaji wa mradi.

Kwa upande wa Tanzania Bomba litapita katika mikoa 8 na wilaya 24 ambapo wilaya ya Kiteto itapitiwa na bomba kwa urefu wa kilomita 117.1 pamoja na ujenzi wa kambi ya kuhifadhi mabomba katika kijiji cha Ndaleta na kambi ya wafanyakazi katika Kijiji cha Njoro.

Tazama video hapo chini