Jumatano , 26th Feb , 2020

Aliyewahi kuwa Katibu wa Uenezi wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA), Edward Simbeye leo Februari 26, 2020, amejivua uanachama ndani ya chama hicho na kusema kuwa atapumzika siasa kwa muda ili aweze kutafakari kwa kina chama chenye malengo ya kweli.

Kushoto ni Mawaziri Wakuu Wastaafu Edward Lowassa na Frederick Sumaye, kulia ni aliyewahi kuwa Katibu Uenezi CHADEMA Edward Simbeye.

Kauli hiyo ameitoa ikiwa ni siku chache tangu aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho Dkt Vicent Mashinji, kujiunga na Chama cha Mapinduzi, ambapo amesema kuwa chama hicho hakina maono yoyote ya baadaye na kwamba chama hicho ni kampuni binafsi kwani kilishindwa kuwaheshimu Lowassa na Sumaye.

"Chama changu kimetoka kwenye malengo ya msingi ya kuchukua dola na kuwa kikundi cha watu wachache na kampuni ya mtu binafsi, wote tunajua ambavyo tumemdhalilisha Sumaye, tulimfukuza Lowassa wenyewe kwa sababu aliingilia maslahi ya mtu mmoja kwenye chama ni vyema tukawaomba msamaha wazee hawa na mimi leo kwa niaba ya wenye akili ninawaomba msamaha" amesema Simbeye.