Jumanne , 15th Mei , 2018

Rais Dkt. John Magufuli amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James kumpandisha cheo Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa wa TRA bandari ya Dar es Salaam Usaje Asubisye na kuwa Kamishna kamili bandarini hapo ndani ya wiki hii.

Dkt. Magufuli ametoa agizo hilo wakati alipokuwa anazungumza viongozi mbalimbali kwenye bandari ya Dar es Salaam mara baada ya kumaliza ziara yake ya kushtukiza kwenye bandari na kusema amefanya hivyo kutokana na kazi nzuri aliyoifanya Ben Usaje katika kusimamia maslahi ya nchi vizuri.

"Nawapongeza watu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kazi nzuri mnayoifanya,  Waziri wa Fedha kampeni tu huyu ukamishna kamili kwa sababu amesimamia haki halisi kwaajili ya maslahi mapana ya nchi yetu, najua wanamchukia sana wengine wafanyabiashara lakini waache wakuchukie Mungu anakupenda na watanzania tutaendelea kukupenda kwa hiyo mka-confirm. Katibu Mkuu mkazungumze wote mumpe angalau ndani ya wiki hii msimcheleweshe", amesema Dkt. Magufuli.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli umekuja baada ya kumuuliza swali Kaimu Kamishna kuwa anafanya kazi gani TRA na ndipo alipotoa amri hiyo ya kupandishwa cheo haraka kutokana na kuwa ameweza kusimamia haki na maslahi kwa ufasaha.