Alhamisi , 30th Mar , 2023

Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera Dk. Abel Nyamahanga amemsimamisha uongozi mwenyekiti wa kambi ya wavuvi - BMU Thobias Masebwe wa  mwalo wa Magarini kata ya Nyakabango, kwa tuhuma ya kuiba zana za uvuvi haramu, ambazo zilikamatwa kwenye doria na kuhifadhiwa katika mwalo huo

Akizungumza wakati wa kuteketeza zana haramu za uvuvi Dk. Nyamahanga amesema kuwa zoezi la ukamataji wa zana hizo limefanyika kwa muda wa miezi mitatu na kwamba ndani ya kipindi hicho doria 28 zimefanyika

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa zana hizo ambazo anatuhumiwa kuziiba mwenyekiti huyo wa BMU, anadaiwa kushirikiana na mjumbe wa kambi hiyo ambaye pia amesimamishwa uongozi

Zana zilizoteketezwa leo ni makokoro 80, nyavu za timba 217, nyavu za makira 320 na tupatupa tatu zote zikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 97.7

Kwa upande wake Afisa uvuvi Wilaya ya Muleba Wilfred Tibendelana amesema kuwa wanaendelea kufanya doria za mara kwa mara upande wa visiwani na nchi kavu, ili kuwabaini watu wanaojihusisha na vitendo vya uvuvi  usiokubalika kisheria, ili waweze kuchukuliwa hatua, lengo likiwa ni kulinda rasirimali za ziwa Victoria.

Nao baadhi ya wananchi katika wilaya hiyo wamesema kuwa vitendo vya uvuvi haramu  vimekuwa vikirudisha maendeleo nyuma na kusababisha samaki kupungua ziwani