Jumatano , 21st Nov , 2018

Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Mbeya, Evarist Chengula amefariki dunia leo asubuhi akiwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alipokuwa anapatiwa matibabu ya moyo.

Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Mbeya, Evarist Chengula enzi za uhai wake.

Askofu Chengula alifika jijini Dar es salaam jana, akitokea Mbeya ambako alikuwa hajazidiwa sana na alifikishwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili kitengo cha Moyo (JKIC).

Akizungumza na www.eatv.tv, Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padre. Charles Kitima amesema kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo yaliyochangiwa na umri wake ambapo amefariki akiwa na miaka 78.

"Baba Askofu hakuwa anaumwa sana lakini alikuwa na tatizo la Moyo ambalo alikuwa analimudu kawaida na alikuwa anaendelea na kazi kama kawaida mpaka Alhamisi iliyopita ameongoza misa takatifu hali ilipobadilika ndipo alimtafta daktari wake", amesema Padre. Kitima.

Padre Kitima amesema kuwa Askofu Chengula atazikwa jijini Mbeya siku ya Jumanne katika kanisa alilokuwa akihudumia Askofu.