Bajeti Kuu ya Shilingi Trilioni 36.33 yawasilishwa

Alhamisi , 10th Jun , 2021

Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, amewasilisha makadario ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ya Shilingi Trilioni 36.33 ambalo ni ongezeko la asilimia 4 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2020/21 ya Shilingi Trilioni 34.87.

Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba

Akisoma hotuba ya bajeti leo bungeni, Dkt. Nchemba ameseme bajeti hiyo imezingatia miongozo mbalimbali ikiwemo mpango wa tatu wa maendeleo ya taifa wa miaka mitano, pamoja na maagizo ya rais hususan katika kudumisha tunu za taifa, kuongeza tija ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, kukuza sekta ya viwanda pamoja na kuziba mianya ya utoroshaji wa madini.

"Mhe. Spika, kwa mwaka 2021/22, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 36.33 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo, kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 23.0 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 13.33 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo,” amesema Dkt. Nchemba.

Ameongeza kwa kusema kuwa “Fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida zinajumuisha shilingi trilioni 10.66 kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali, shilingi trilioni 8.15 kwa ajili ya mishahara na shilingi trilioni 4.19 kwa ajili ya matumizi mengineyo. Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 200.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, wazabuni na watoa huduma".

Waziri Dkt. Nchemba ameeleza tathimini za bajeti iliyopita ya mwaka 2020/21 ambapo serikali ilijipanga kukusanya shilingi trilioni 34.88 kutoka kwa vyanzo vya mapatao vya ndani na nje ya nchi, lakini hadi kufikia Aprili 2021 tayari shilingi trilioni 24.53 zimekusanywa sawa na asilimia 86.1.