Alhamisi , 26th Mar , 2020

Balozi wa Kenya nchini Tanzania , Balozi Dan Kazungu, amewataka Wakenya wote waishio nchini kuhakiksiha wanafuata taratibu zote zinazotolewa na wataalam wa afya kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa hatari unaosababishwa na Virusi vya Corona.

Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu

Balozi Kazungu ameyabainisha hayo leo Machi 26, 2020, wakati wa ziara yake maalum katika kituo cha runinga cha EATV, ambapo amesema kuwa ugonjwa huo ni hatari na kwamba unaeneo kwa haraka zaidi.

"Kenya ilitangaza kesi ya kwanza kwa mtu mwenye Corona Machi 13, 2020, ningependa kuwashauri ndugu zangu kuchukua tahadhari tuliyopewa na Shirika la Afya Duniani juu ya ugonjwa huu, tunatakiwa kuosha mikono yetu kwa sabuni, kutumia sanitizer, tuepuke kushikana mikono, tuepuke kugusa midomo na pua zetu, ambavyo vitasababisha kupata virusi kwa haraka" ameeleza Balozi Kazungu.

"Tuepuke mikusanyiko ya watu kwa vyovyote itakavyowezekana, tuwe wasafi, tupeane umbali kidogo na mtu, kukaa nyumbani kama utakuwa na dalili kama kukohoa na mafua, kisha chukua vipimo ili kujua tatizo" ameongeza.