Jumapili , 9th Dec , 2018

Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) wameadhimisha siku ya Uhuru kwa kuwatembelea viongozi wa chama hicho walioko gereza la Segerea huku wakikosoa uamuzi wa kufutwa kwa sherehe hizo.

Mwenyekiti wa BAVICHA Patrick Olesosopi, akisisitiza jambo.

Akizungumza leo Desemba 9, Mwenyekiti wa Bavicha Patrick Olesosopi amesema siku ya Uhuru ni muhimu kwa taifa katika kuwakumbuka waasisi waliopigania Uhuru.

"Baada ya kufutwa kwa sherehe za Uhuru sisi kama Bavicha kwa pamoja tuliazimia kujitokeza katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutembelea watu walioko magerezani," amesema Sosopi.

Amesema kwa kuwa sherehe za Uhuru ni muhimu, Rais angeangalia sherehe nyingine za kufuta ikiwamo kupunguza siku za kukimbiza mwenge ili kuokoa fedha ambazo matumizi yake sio ya lazima lakini sio siku ya uhuru.

Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na muweka hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho Ester Matiko wako gereza la Segerea kwa siku ya 14 baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana Novemba 26.