Jumatano , 5th Oct , 2022

Wakulima wa maeneo ya Chikuyu, Maweni na Kintinku wilayani Manyoni mkoani Singida, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan na serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Kilimo kwa mikakati ya ujenzi wa miradi mipya ya umwagiliaji na ukarabati wa miradi ya zamani wilayani humo.

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde

Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde katika miradi ya umwagiliaji katika maeneo hayo na kupata nafasi ya kukagua skimu hizo pamoja na kuongea na wakulima kuwakikishia azma ya serikali kuona skimu zote hizo zinafanya kazi ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na kukuza uchumi wa wakulima.

"Mh Rais Samia anayo dhamira kubwa ya kumuona mkulima wa Tanzania ananufaika na kilimo chake kwa kulima kwa tija na kuongeza kipato kupitia kilimo cha uhakika cha umwagiliaji na ameelekeza eneo la Mbwasa, Manyoni kujengwa bwawa lenye thamani ya bilioni 20 lenye uwezo wa kuhifadhi maji kwa mita za ujazo milioni 10 pamoja na skimu za umwagiliaji katika eneo hilo," amesema Naibu waziri Mavunde

Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo yaliyojitokeza, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, amesema kwamba Tume imejipanga kuhakikisha miradi yote mipya ya skimu za umwagiliaji inakuwa na chanzo cha uhakika cha maji ili kuruhusu shughuli za kilimo cha umwagiliaji kufanyika zaidi ya mara moja kwa mwaka.