Alhamisi , 17th Oct , 2019

Baada ya Mahakama ya Rufaa kutengua hukumu iliyowazuia wakurugenzi kusimamia uchaguzi, Mwanaharakati Bob Chacha Wangwe ameeleza nia yake ya kukatia rufaa maamuzi hayo katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu ili kuhakikisha demokrasia inapatikana.

Bob Chacha Wangwe

Akizungumza leo Oktoba 17, 2019 na EATV&EA Radio Digital, Bob Chacha Wangwe amesema kuwa hadi sasa wameshaanza kuandaa utaratibu wa kukata rufaa nje ya Tanzania kwa kile anachokiamini kuwa kama haki imeshindwa kupatikana nyumbani, basi ataipata nje ya nchi.

''Ushindi huo wa upande wa Serikali tumeupokea kwa masikitiko makubwa kwasababu tunategemea demokrasia iendelee, tunapoona inarudi nyuma ni jambo ambalo linasikitisha. Sisi tutakata rufaa kwenda mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu kwa sababu kwa Tanzania mahakama ya rufaa ndiyo mahakama ya juu zaidi", amesema Wangwe.

"Kwahiyo inapotokea imetoa uamuzi sisi hatuwezi tukarudi nyumbani, tunapoona hatujatendewa haki inabidi tukaitafute hiyo haki ambayo tumeikosa'', ameongeza.

Jana Oktoba 16, 2019, Mahakama ya Rufani Tanzania ilitengua hukumu na amri ya Mahakama Kuu kuzuia wakurugenzi wa halmashauri, manispaa, na majiji kusimamia Uchaguzi Mkuu kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.