Jumatano , 6th Mei , 2015

Zoezi la uandikishaji wananchi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura katika kata ya Ruaha manispaa ya Iringa linaendelea vizuri ambapo linatarajiwa kukamilika kesho.

Mmoja wa Wananchi waliojitokeza kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga kura kwa mfumo wa BVR.

Afisa mtendaji wa kata ya Ruaha Bi. Bahati Mlatu amesema zoezi hilo linakwenda vizuri licha ya kuwepo changamoto za kawaida hususani alama za vidole kutokusoma kwenye mashine za BVR.

Naye wakala wa uandikishaji kutoka chama cha mapinduzi (CCM) katika kituo cha Kwamwagongo eneo la Ipogolo Bi. Jane Myovela amesema zoezi linakwenda vizuri.

Valentina Mfalamagoha na Lucy Nyaulingo ni miongoni mwa wananchi wa kata ya Ruaha wameridhishwa na zoezi hilo.

Katika kata ya Ruaha kuna vituo 13 ambavyo vinaendesha zoezi la uandikishaji ambavyo ni Ipogolo A, B, C, D na E, Kinegamgosi A, B na C, Buguruni, Ngereli, Kwamwagongo, Chuo cha CDTI na Tagamenda.

Hata hivyo, afisa mtendaji wa kata ya Ruaha Bi. Bahati Mlatu amewashauri wananchi kujitokeza katika zoezi hilo ili kupata vitambulisho vya kupigia kura ambavyo ni haki yao ya kikatiba.