Alhamisi , 26th Mar , 2015

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) MKoani Arusha, Robson Meitinyiki, amemtaka Katibu wa halmashauri Kuu (Nec) Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kuchunga kauli zake dhidi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa

Hayo ameyasema leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya kauli ya Nape dhidi ya Lowassa kuwa, amepoteza sifa ya kuwa mgombea wa uraisi kupitia chama hicho kwa kuyatuma makundi mbalimbali kujifanya yanamshawishi kuchukua fomu.

Amesema anapaswa kuelewa chama hicho kilibomoka na ni chama cha watu wote na kwa sasa chama kimeanza kuimarika kupitia jitihada za Katibu Mkuu, Abdurahamani Kinana na yeye anaanza kujinyanyua na kutaka kukibomoa.

Robson amesema Nape aelewe nyuma ya Lowassa wapo wengi na Arusha wanajipanga kwenda kumshawishi achukue fomu na yeye hapaswi kutoa maneno ya kejeli, kwani kuna kanuni na taratibu za vyama vya kumsimamisha mtu kuwa mgombea, kama ana mgombea wake amtangaze japo lazima apitishwe na chama,siyo mtu mmoja.

Aidha amesema kama Edward Lowassa anafanya maigizo, ili apendwe na watu, basi wanamshauri mgombea wa Nape afanye maigizo hayo, ili apendwe na watu kwa kufuatwa nyumbani kwake.

Amesema Nape aache watu wamfuate Lowassa na kumshawishi kwani sauti ya watu wengi ni sauti ya Mungu na pia Mwenyekiti taifa alishasema watu wamshawishi,na kauli zake zinaturudisha nyuma kutekeleza maagizo ya Kinana aliyowaachia,kukijenga chama.

Naye Katibu Mwenezi Mkoa wa Arusha, Isack Joseph,Amesema Nape afike mahali achunge kauli zake dhidi ya Lowassa, kwani Lowasa ni mtu mwenye heshima katika nchi hii na alikuwa Waziri Mkuu na kuiletea taifa heshima kubwa, hivyo vema vikao ya CC na NEC viachiwe viamue.

Amesema Kinana ameweka heshima kwa chama na kuondoa dhana ya kutoleana heshima ya kupachikana majina ya magamba na sasa chama kimerudi kwenye chati yeye Nape anataka kurudisha nyuma.