CCM kuziba nafasi za viongozi waliotimkia UKAWA

Jumanne , 9th Feb , 2016

Kamati kuu ya chama cha Mapinduzi CCM imefanya uteuzi mpya wa nafasi za uenyekiti zilizoachwa wazi kati ngazi ya mikoa na wilaya ambapo viongozi hao walijiunga na Vyama vya Upinzania pamoja na wengine kufariki dunia.

Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM

Akiongea na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho Mhe. Nape Nnauye amesema uteuzi huo umetokana na vifo pamoja na baadhi ya viongozi kuhamia vyama vya upinzani wengi wao wakihamia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Nape amesema mikoa mitatu wenyeviti wake walihama imeshapata wagombea wa nafasi hizo ambapo ni mkoa wa Shinyanga alipokuwepo mwenyekiti Khamis Mgeja, Arusha, Onesmo Ole Nangole, na Mgana Msindai wa Singida ambao wote walihamia UKAWA.

Mhe. Nape aliwataja wagombea wa nafasi hizo zilizoachwa wazi kuwa ni Michael Lekule, Emanuel Lusenga na John Pallangyo uenyekiti Arusha, Mkoa wa Shinyanga ni Hassan Mwendapole, Mbala Mlolwa na Eraso Kwilasa (Uenyekiti), Mkoa wa Singida, Hanje Barnabas, Misanga Hamis, Martha Mlata na Kilimba Juma (Uenyekiti).

Aidha Nape amesema nafasi nyingine zilizojazwa ni pamoja na Katibu wa Uchumi na Fedha Mkoa wa Kilimanjaro, Katibu wa siasa na uenezi Mkoa wa Arusha na uenyekiti wa vijana CCM, mkoa nazo zitazibwa,

Mbali na hizo nafasi nyingine ambazo zitazibwa baada ya kuachwa wazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya viongozi kuihama CCM na vifo ni zile za ujumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM, Taifa na uenyekiti wa CCM wilaya.