Jumapili , 21st Mei , 2023

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imeielekeza serikali kufanya uchambuzi wa kina wa masuala yaliyoibuliwa na kulalamikiwa na wafanyabiashara wa Kariakoo ili kutafuta kiini cha tatizo hilo na kutafutia ufumbuzi wa kudumu.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan, wakati akiongoza kikao maalum cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa

Hayo yamebainishwa leo Mei 21, 2023, na Kamati Kuu hiyo wakati ikijadili kwa kina taarifa kuhusu mgogoro wa wafanyabiashara wa soko la kimataifa la Kariakoo uliotokea hivi karibuni waliokuwa wakilalamikia masuala ya kikodi.

Aidha serikali imeelekezwa kuhakikisha inatengeneza utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu wa changamoto zinazoibuka kote nchini ili kuhakikisha hazileti madhara kama yaliyotokea Kariakoo.

Kamati hiyo imetoa maelekezo hayo katika kikao chake maalum kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan baada ya kupokea na kujadili taarifa kuhusu mgogoro wa wafanyabiashara wa soko hilo.

Wafanyabiashara wa Kariakoo waligoma kufungua biashara zao kwa takribani siku tatu, hadi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipoingilia kati na kukutana nao na kuweka maazimio ikiwemo kuunda kamati ya watu 14 ambayo itachunguza changamoto zote zinazowakabili wafanyabiashara nchini, na kuzuia baadhi ya mambo ikiwemo shughuli ya kikosi kazi kutoka TRA kilichokuwa kikiwasumbua wafanyabiashara hao.