Jumatatu , 25th Nov , 2019

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, amesema kati ya Vijiji 12,262  Chama Cha Mapinduzi, kimefanikiwa kushinda Vijiji 12,260 huku vyama vya CHADEMA na CUF, vyenyewe vikifanikiwa kushidna Kijiji kimoja kimoja.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo.

Waziri Jafo ametoa kauli hiyo leo Novemba 25, 2019, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusiana na zoezi la Uchaguzi ambalo limefanyika jana Novemba 24, katika mikoa mbalimbali nchini, ambapo CCM imefanikiwa kuibuka mshindi wa uchaguzi huo kwa kushinda maeneo mengi zaidi.

"Kwenye Uenyekiti wa Kijiji CHADEMA imeshinda nafasi 1, haikufanikiwa kupata Mtaa, CUF wameshinda nafasi 1 ya Uenyekiti wa Kijiji, Mtaa hawajapata hata mmoja, ACT Wazalendo haikupata Mwenyekiti wa Kijiji wala Mtaa", amesema Waziri Jafo.

Aidha Waziri Jafo ameongeza kuwa, "Kulikuwa na Vijiji 12,262 Mitaa 4,263, CCM imeshinda Vijiji 12,260 sawa na asilimia 99.99, kimeshinda Mitaa 4,263 sawa na asilimia 100.

Katika Uchaguzi huo baadhi ya vyama vya upinzani nchini, vilitangaza kutoshiriki katika kinyang'anyiro hicho kwa madai ya kwamba, hakukuwa na uwanja sawa kwenye kupitisha wagombea.