
Akizungumza kwa njia ya mtandao na Baraza la Kidigitali la chama hicho leo Septemba 2, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyasa ameeleza sababu kuu ni kuwaenzi mashujaa hao kutokana na mchango wao katika kupigana haki na kudai demokrasia.
Katibu Mkuu wa CHADEMA kanda ya Nyasa, Grace Shiwo amesema kuwa kanda ya Nyasa imepata misukosuko ya muda mrefu tangu tukio la mwanahabari Daudi Mwangosi la mwaka 2011 hadi sasa huku akitaja baadhi ya mashujaa wa Chama hicho.
“Daudi Mwangosi alikuwa ni mwandishi wa habari aliyepigwa na bomu mwaka 2011 huko Nyororo wakati wa ufunguzi wa ofisi za chama naalipoteza maisha. Kule Njombe kuna George Sanga ambaye alipewa kesi ya mauaji yeye pamoja na wenzake mnamo 2020 na hivyo kukaa gerezani kwa muda mrefu na familia zao kuathirika kiuchumi hadi Disemba 2024.”
Amemtaja Joseph Mbilinyi na Kamanda Mdude ambaye alichukuliwa na watu waliojitambulisha kuwa ni maaskari na kupigwa na kitu kizito kiasi cha kuvuja damu na hajapatikana mpaka sasa. Pia ametaja kuhusu Steven Chalamila aliyeuliwa wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa pamoja na mashujaa wengine.
Aidha, kuelekea kilele cha maadhimisho hayo makatibu na wenyeviti hao wa kanda mbalimbali wamesema kuwa kuanzia kesho Jumatano, Septemba 3 watavaa mavazi ya rangi nyekundu ili kuenzi mchango wao katika kupigania haki nchini.