Jumapili , 5th Jul , 2020

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika, ametoa rai kwa wanachama wote wa chama hicho, hata wale ambao hawakutia nia za kugombea nafasi mbalimbali ikiwemo Urais, wajitokeze kwa ajili ya kwenda kuchukua fomu za kuwania uteuzi ndani ya chama.

Bendera za CHADEMA.

Taarifa hiyo imetolewa leo Julai 5, 2020 na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho Tumaini Makene, ambapo imeeleza kuwa Mnyika ametoa rai kwa wananchi kuwa wahakikishe mgombea atakayeshinda uchaguzi anatangazwa kwa nguvu ya umma.

"Natoa wito kwa wanachama hata wale hawakutia nia, waende kwenye ofisi za chama wakachukue fomu, kutia nia ni jambo moja na kuchukua fomu ni jambo lingine, kwa ujumbe huu nawataarifu wanachama wote kutumia fursa hii ili mteuliwe muende kuwahudumia wananchi" imeeleza taarifa hiyo.

Aidha akitoa taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya kujiandaa na Uchaguzi Mkuu Naibu Katibu Mkuu Bara, Singo Kigaila, amesema kuwa jumla ya wanachama 148 wametia nia kwenye nafasi ya Ubunge kwenye majimbo 19 ya kanda hiyo, huku madiwani waliotia nia wakiwa 691.