DC akanusha kuagiza bendera za CHADEMA kushushwa

Jumatatu , 9th Dec , 2019

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Dkt Khalfan Haule, amekanusha taarifa zinazotembea kwenye mitandao ya kijamii kuwa yeye aliagiza bendera zote za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika wilaya yake kung'olewa.

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dkt Khalfan Haule.

Dkt Haule amesema kuwa taarifa hizo si za kweli, bali yeye aliagiza kuwa bendera zote za CHADEMA ambazo wagombea wake hawakuchaguliwa, zitolewe na zisimamishwe zile bendera ambazo viongozi wake walichaguliwa, kupitia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika hivi karibuni.

"Katika mazungumzo yetu na viongozi wa Serikali za Mitaa, ilionekana viongozi wa CHADEMA wale waliomaliza muda wao bado wanapeperusha bendera kwenye maeneo yao na bado wanawahudumia wananchi, tulikubaliana kuwa ni busara kwamba kwa vile wao sasa sio viongozi, ni busara kuondoa bendera pale na kuwaelekeza wananchi waende kupata huduma kwa viongozi waliochaguliwa sasa hivi, hakuna mahala ambapo nilisema ni lazima" amesema DC Haule.

Kauli hiyo ya kuagiza bendera za CHADEMA zitolewe aliitoa juzi Desemba 7, 2019, wakati wa mkutano wake na viongozi wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji waliochaguliwa hivi karibuni.