Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir, ametangaza rasmi kuwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani utaendelea kwa siku ya kesho baada ya mwezi kutoandama katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa taarifa hiyo leo, amebainisha kuwa kutokana na kutofikiwa kwa vigezo vya kuonekana kwa mwezi, waumini wa dini ya Kiislamu wanapaswa kukamilisha idadi ya siku za mfungo kabla ya kusherehekea Sikukuu ya Eid el-Fitri.
Kufuatia tangazo hilo, Mufti amewataka Waislamu kote nchini kutumia muda uliobakia kuongeza ibada, kutoa sadaka, na kudumisha amani pamoja na mshikamano.
Amesema kuwa kukosekana kwa taarifa za kuandama kwa mwezi ni sehemu ya taratibu za kisheria za kidini, hivyo amewasihi waumini kuwa watulivu na kusubiri maelekezo rasmi kuhusu siku ya kuanza kwa sherehe za sikukuu hiyo baada ya kukamilika kwa mfungo.





