Alhamisi , 12th Mei , 2016

Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Ally Salum Hapi amewataka maofisa usalama katika wilaya yake kuchukua hatua mara moja ya kuimarisha ulinzi katika maeneo ya Manzese ambako kuna lalamikiwa na wananchi kwa kukidhiri ualifu, ubakaji na madadapoa.

Akiongea katika oparesheni aliyoifanya katika maeneo mbalimbali ya Manzese Mkuu wa wilaya hiyo amesema wananchi wamempa taarifa juu ya uhalifu wa kila siku unaofanyika Manzese na biashara ya ngono inayoendelea na kuwataka maofisa hao kuchukuwa hatua za haraka kuzuia uhalifu huo.

Aidha, katika ukaguzi huo pia Mhe. Hapi ameagiza kukaguliwa kwa leseni ya wafanyabiashara wawili katika maeneo hayo ambao mmoja alikuwa akiendesha ghala bila kibali cha kufanya hivyo na kukutwa na magunia ya sukari ndani yake pamoja na mmiliki wa nyumba ya kulala wageni (Guest House) inayoatarisha afya ya watumiaji wake.

Nyumba hiyo ya kulala wageni iligundulika kuwa na mapungufu mengi ya kimazingira, utiririshwaji wa majitaka, juu ya ukumbi wa disko ni eneo la kisima ambalo pia limetajwa kuhatarisha maisha ya watumiaji wake jambo ambalo limemlazimu mkuu huyo wa wilaya kutaka hatua za haraka kuchukuliwa.

Wakazi wa maeneo hayo walipokuwa wakihojiwa na mwandishi wetu kuhusiana na nyumba hiyo ya kulala wageni walieleza kuwa gesti hiyo ni maarufu kwa madadapoa, shuguli za ukahaba zinafanyika hapo huku wakieleza malipo yake kuwa shilingi elfu 8 kwa VIP na shilingi elfu tatu kwa shorttime na bei inapungua ukilalamika.

Wengi wa wakazi waliofurika kushuhudia ukaguzi huo wamesema heri gesti hiyo ifungiwe, kwani inauchafu mwingi unaotendeka. Miliki wa nyumba hiyo Vaines Mrema maarufu kama Mama Rambo alimueleza kuwa nyumba yake imekuwa ikifanyiwa ukaguzi na afisa afya wa ngazi ya mtaa licha ya mapungufu lukuki yaliyobainika.