Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amewasili mapema Jumatano na kupokelewa na waziri wa mambo ya kigeni Alfred Mutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA. Ajenda ya ziara ya Guterres inajikita katika mzozo wa Sudan iliyotumbukia kwenye vita tangu katikati ya Aprili mwaka huu. Akizungumza jijini Nairobi, Guterres ameusisitizia umuhimu wa risasi kukoma kurindima Sudan.
Wakati wa mchana, Katibu Mkuu huyo amekutana na wafanyakazi wake katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa iliyoko jijini Nairobi, UNON alikofanya kikao na waandishi wa habari. Kadhalika amehudhuria mkutano wa kwanza wa uratibu wa maafisa wakuu watendaji wa Umoja wa Mataifa
Ziara ya Antonio Guterres itampeleka pia hadi eneo la maziwa makuu atakakohudhuria mjini Bujumbura, kongamano la 11 la viongozi wa ngazi ya juu wa uangalizi wa mifumo ya amani,usalama na ushirikiano mintarafu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na eneo zima.