Licha ya Tanzania kuwa na idadi kubwa ya mifugo, bado inalazimika kutumia zaidi ya Sh23 bilioni kila mwaka kuagiza wastani wa lita milioni 11.6 za maziwa kutoka nje ya nchi hali inayochangiwa na changamoto za ubora ambapo miundombinu na elimu kwa wadau wa sekta maziwa ni vikwazo vinavyosababisha maziwa kukosa ubora.
Akizungumza katika mafunzo ya wakaguzi wa tasnia ya maziwa mjini Morogoro, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Profesa George Msalya amesema licha ya Tanzania kuzalisha takribani lita bilioni 4.1 za maziwa kwa mwaka, bado kuna pengo la uzalishaji linalosababisha nchi kuendelea kuagiza maziwa kutoka nje ili kukidhi mahitaji ya ndani.
Profesa Msalya amesema changamoto kubwa ni ubora wa maziwa yanayozalishwa na wadau wengi, hasa wa vijijini, hawazingatii viwango vinavyotakiwa, hali inayowafanya walaji wengi kuamini kuwa maziwa ya nje ni bora zaidi kuliko yanayozalishwa nchini.
Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania ina jumla ya viwanda 188 vya kusindika maziwa, vikiwemo vidogo, vya kati na vikubwa, lakini ni vinane pekee vilivyo katika kundi la viwanda vikubwa.


