Alhamisi , 10th Oct , 2019

Mfanyabiashara Harbinder Sethi, leo Oktoba 10, 2019, kupitia Wakili wake Michael Ngalo, amemuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kukiri makosa yake ya uhujumu uchumi, ambapo kwa sasa yuko tayari kuomba radhi.

Hayo yamejiri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi, wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Seth na mwenzake James Rugemalira, wanakabiliwa na mashtaka 12 wanayodaiwa kuyatenda hapa nchini na mengine nje ya nchi, ikiwemo Kenya na India, ikiwemo kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, utakatishaji wa fedha na kuisababisha Serikali, hasara ya zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 22, pamoja na Shilingi bilioni 309.

Harbinder Seth na Rugemalira, walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza June 19, 2017, ambapo kwa kipindi chote hicho, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwa mujibu Wakili wa Serikali Wankyo Simon, amesema hawezi kuahidi kama utaweza kukamilika lini, ambapo kesi hiyo imeahirishwa tena hadi Oktoba 24, 2019.