Jumatatu , 14th Oct , 2019

Aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Stephen Wasira amezungumza jinsi kipindi cha miaka 7 ya Ukuu wa Mkoa wa Mara ulivyomsaidia kumfahamu vizuri hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Stephen Wasira

Wasira ameyabainisha hayo leo Oktoba 14, 2019, wakati wa Kongamano la kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa, lililofanyika Kijijini Butiama mkoani Mara.

''Kama kuna wakati nimejifunza juu ya maisha ya Mwalimu ni katika kipindi cha mika 7 na nusu ya Ukuu wa Mkoa wa Mara kwasababu alikuwa anakuja hapa kila Pasaka na Christmas, anakaa sana na kiserikali mimi ndiye nilikuwa mwenyeji wake, Mwalimu alikuwa anasikiliza sana hata kama unaongea vitu vya hovyo hovyo anakusikiliza na wala hakuambii ukae'', amesema Wasira.

Aidha Wasira amelizungumzia suala la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila la kuwachapa Wanafunzi viboko akisema kuwa hata Mwalimu aliwahi kufanya hivyo kwa kina hayati Samuel Sitta walipokuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu.

''Nchi inaendeshwa kwa utaratibu, kama utaratibu ni viboko wanachapwa tu, maana hata Mwalimu alishawahi kuwachapa kina Sitta viboko pale Ikulu, wakiwa Wanafunzi wa Chuo Kikuu, walijifanya vituko aliwachapa mwenyewe, aliuvua Urais akawa Mwalimu, inategemea hali ilivyo kwa wakati huo'', ameongeza.

Wasira ameendelea kumsifia Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kwamba alikuwa ni mtu anayechukia umaskini na hakutaka huo utajiri awe nao peke yake na kwamba kama angetaka hivyo huenda ndiyo angekuwa ni tajiri mkubwa Afrika na Duniani.