Ameyasema hayo wilayani Ushetu mkoani Shinyanga, mara baada ya kutembelea Kata ya Mlowa wakati wa ziara yake kikazi yenye lengo la kutatua changamoto baina ya wananchi na wahifadhi.
"Sisi tumepewa dhamana ya kusimamia maliasili kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo, katika kutekeleza jukumu hili hatupaswi kuleta taharuki kwa wananchi," amesisitiza Naibu Waziri Masanja
Amewaeleza wananchi hao kuwa mtu yeyote anapovunja sheria kwa kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa bila vibali lazima utaratibu wa kisheria ufuatwe ikiwemo kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi hao waendelee kufuata sheria na kuacha kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa kwa kuwa maeneo hayo ni muhimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Pia, amewataka Askari Uhifadhi waandae programu za kutoa elimu kwa wananchi ili wajue umuhimu na faida za uhifadhi ikiwemo kuleta mvua, kutunza vyanzo vya maji,kuchavusha mazao na kusaidia katika masuala ya ulinzi na usalama wa nchi.

