Jumamosi , 11th Feb , 2023

Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wanafunzi na watanzania kuacha kuiga baadhi ya mambo ya nje ya nchi ambayo yanakwenda kinyume na mila na tamaduni za mtanzania huku akiwataka vijana kuwalinda wadogo zao kwa hali sio swari

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Feb 11/2023 wakati akizungumza na Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) na Zanzibar (TAHLIFE) jijini Dodoma

"Lindeni wadogo zenu vinginevyo mtakuja kuwa na taifa la ajabu, huko tunakotembea nje mambo sio swari, tuishini kwa mila na desturi zetu, mambo ya kuletewa yapo ya kuiga, suti zimetoka nje tunavaa tunapendeza, unataka kusema kizungu cha kubana pua sema, lakini yale mengine acha" amesema Rais Samia

Aidha katika hatua nyingine Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Elimu kuyatoa majengo yanayotumika na wizara hiyo kwa sasa kwenda TAHLISO mara tu wakatapohamia katika majengo mapya ya Wizara hiyo yanayojengwa Mtumba Jijini Dodoma 

"Nitoe maelekezo kwa waziri wa elimu kwamba najua karibu mnamaliza majengo yenu pale Mtumba, kwahiyo mtakapohamia mtumba yale majengo mnayotumia sasa myakabishi kwa TAHLISO"

Rais Samia ameahidi kutoa samani na vitendea kazi vya ofisi za Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) na Zanzibar (TAHLIFE)