"Ibada zikifungwa, watu watakufa" - Gwajima

Jumatatu , 23rd Mar , 2020

Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima amesema kuwa hakuna haja ya watu kufanya ibada kwa njia ya mitandao ya kijamii kama wanavyofanya wengine kwakuwa, watu wengi ni maskini na faraja yao wanaipata kanisani.

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Askofu Gwajima ameyabainisha hayo kupitia mazungumzo maalum aliyofanya na EATV&EA Radio Digital, wakati akijibu swali la kwamba haoni kama kuna haja ya yeye kuanzisha maombi kwa njia ya mitandao ili kuepusha misongamano ya watu katika kipindi hiki ambacho Dunia inapambana na ugonjwa hatari unaosababishwa na Virusi vya Corona.

"Ni hatari sana kwa sababu watu wetu sisi ni maskini, kanisani ni mahala pa faraja ambapo watu wanapewa, tukisema tufunge kuabudu watakufa watu wengi sana na kuna uvumi kuwa ugonjwa huu hauna dawa ukiupata unakufa, sisi tukikutana nao tutawaelimisha kwamba ukipata hautakufa" amesema Gwajima.

Mpaka sasa nchi ya Tanzania ina jumla ya wagonjwa 12 wenye maambukizi ya Virusi vya Corona.