Alhamisi , 29th Apr , 2021

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amewataka watu wanaopata msamaha wa vifungo kutoka gerezani kuacha kujihusisha na uvunjifu wa amani, ikiwa pamoja na kuacha kujiingiza tena kwenye matukio ya uhalifu na badala yake wajikite katika kuleta maendeleo kwenye jamii.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro

IGP Sirro amesema hayo leo wakati akizindua kitabu cha muongozo wa kufichua na kuzuia uhalifu ,kitabu ambacho kinalenga kutoa dira hasa katika utekelezaji wa mpango wa Polisi  kupitia mpango mkakati wa ushirikishwaji wa jamii.

“Nitoe angalizo kuna baadhi ya wahalifu wametoka magereza siku za karibuni ambao baada ya vifungo vyao wamesamehewe na Mhe. Rais, kuna baadhi ya matukio ambayo kwetu tulikuwa tumeanza kuyasahau yameanza kurudi tena kwa nguvu kubwa, niwaombe hao ambao hawataki kubadilika, kama hutaki kubadilika na familia yako imeshindwa kukubadilisha au jamii usijelaumu serikali,” amesema IGP Sirro

Aidha IGP Sirro amewaomba watanzania kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kuhusiana na vitendo vya uhalifu ,huku akiwaonya wale wanaojikita katika kutelekeza matukio ya uhalifu kuwa jeshi la polisi halitokaa pembeni bali litatekeleza wajibu wake.