Ijumaa , 23rd Aug , 2019

Wakili wa  kujitegemea Albert Msando, amekabidhi kiasi cha Shilingi milioni tano kama mchango wa kumsaidia kumlipia deni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, alilokuwa  anadaiwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Rais Magufuli

Deni hilo lilikuja baada ya Rais Magufuli, kufika hospitalini hapo kwa lengo la kuwatembelea majeruhi wa ajali ya moto Mkoani Morogoro, alijitokeza  mwanamke aliyemuomba msaada wa kumlipia gharama za matibabu,  baada ya mama yake kufariki dunia, ambapo Rais Magufuli aliuagiza uongozi wa hospitali hiyo kumuachia na kwamba yeye atazilipa gharama hizo.

''Mimi binafsi kupitia akaunti yangu ya instagramu niliamua kuwahamasisha wananchi wamchangie Rais Magufuli ili tuweze kulipa hili deni, lengo la kufanya hivi ni kuhamasisha matumizi bora ya mitandao ya kijamii, jambo la pili nikuonyesha kwamba Mh Rais na yeye ni binadamu kama alivyo mwingine ambaye na yeye anaguswa na ndio maana siku zile alisema Profesa nidai mimi'', amesema Msando.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Muhimbili Profesa Laurence Museru,  amesema kufuatia agizo la Rais Magufuli la wao kumruhusu mwanamke huyo kuchukua mwili wa mpendwa wake na kuondoka,  wao kama hospitali walitii agizo hilo na kisha wao kuipeleka bili ya deni hilo Ikulu ya Dar es Salaam.