
Katika operesheni ya kiintelijensia iliyofanyika usiku wa kuamkia leo Agosti 24, 2025 kusini mashariki mwa Iran, maafisa wa usalama wamefanikiwa kuzuia jaribio kubwa la kigaidi lililokuwa likipangwa na kikundi cha wapiganaji wa kigeni baada ya mapambano yaliyodumu kwa saa kadhaa, magaidi sita wakiuawa na wawili wakikamatwa wakiwa hai huku maafisa watatu wa usalama wa Iran wakijeruhiwa wakati wa operesheni hiyo.
Taarifa kutoka Idara ya Usalama ya Mkoa wa Sistan na Baluchestan imeeleza kuwa kikundi hicho kilikuwa na lengo la kushambulia kituo muhimu cha taifa kilichopo mashariki mwa Iran.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, magaidi hao saba ambao si raia wa Iran walivuka mpaka wa mashariki hivi karibuni na kuingia nchini wakiwa na silaha nzito, zikiwemo bunduki za kisasa aina ya M4 na M16, RPG zenye miongozo ya laser, mabomu ya mkono, vesti za mabomu na vifaa vya mawasiliano. Vikosi vya usalama vilifanikiwa kuwafuatilia na kuwakabili kabla hawajatekeleza hujuma walizopanga.
Idara ya Usalama imeeleza kuwa mbinu zilizotumiwa na kikundi hicho zinafanana kwa karibu na zile zinazohusishwa na shirika la ujasusi la Israel, Mossad, jambo linaloibua maswali kuhusu ushawishi wa mashirika ya kigeni katika machafuko ya eneo hilo.
Mkoa wa Sistan na Baluchestan, unaopakana na Pakistan, umeendelea kuwa kitovu cha mashambulizi ya kigaidi katika miaka ya hivi karibuni. Mnamo Oktoba 26 mwaka jana, maafisa kumi wa usalama waliuawa katika shambulizi lililodaiwa na kikundi cha Jaish al-Adl, ambacho kinahusishwa na mashirika ya kijasusi ya nje yanayolenga maslahi ya Iran.