Alhamisi , 23rd Apr , 2026

Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa matukio ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman, ameanika mbinu zilizotumiwa na waratibu wa ghasia kuwaribuni vijana na makundi yenye kipato duni ili kuchochea vurugu nchini.

 

Akiwasilisha ripoti hiyo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Aprili 23, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, Jaji Chande amesema uchunguzi umebaini kuwepo kwa mipango iliyosukwa kwa siri kuanzia katikati ya mwezi Oktoba mwaka jana.

Jaji Chande ameeleza kuwa watu waliohusika na uratibu wa vurugu hizo walipita mitaani kuwashawishi watoto wanaoishi katika mazingira magumu, waendesha pikipiki (Bodaboda), na wajasiriamali wadogo (Machinga) kushiriki kwenye ghasia hizo.

"Kuna Watu walipita Mitaani kuwashawishi Watu kuwaandikisha kufanya vurugu, mfano Watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, waendesha pikipiki na Wajasiriamali wadogo walieleza kuwa walipewa pesa kati ya Tsh. elfu 10,000 hadi elfu 50,000 na kuahidiwa ajira na Maisha bora" alisema Jaji Chande.