Jumapili , 27th Mar , 2016

Watanzania na jumuiya ya kimataifa wametakiwa kuamini kuwa hali ya Zanzibar ni shwari na imetawaliwa na amani na utulivu.

Ujumbe huo umetolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Zanzibar Augustino Shao katika ibada ya sikukuu ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Parokia ya Minara Miwili visiwani Zanzibar.

Askofu Shao amesema kwa sasa wazanzibari hawahitaji kulindwa wala hawahitaji kuishi kwa hofu, kwa kuwa wana uwezo wa kulinda amani waliyonayo wao wenyewe.

Ujumbe huo unafuatia hofu ya kuvurugika kwa amani visiwani humo, ambayo imekuwepo kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa marudio viwani humo.

Aidha katika hatua nyingine, Askofu Shao amewataka wakristo nchini kutumia sikukuu ya Pasaka kwa kutenda haki kwa kila mtu, huku akiviasa pia vyombo vya utoaji haki nchini kuzingatia haki kwa kila mtu bila upendeleo.

Kwa kutumia siku hii, pia amewaasa wakristo kubadili mienendo yao kwa kuacha kutenda maovu ili kumpokea Yesu Kristo ambaye amefufuka leo kwa mujibu wa imani ya kikristo.

Amewaasa watanzania wote kusherehekea Pasaka kwa amani na kwa kusaidia majirani wasiojiweza.