Ijumaa , 23rd Oct , 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewahikikishia watanzania kuwa uchaguzi utakuwa huru na wa amani na wasiwe na hofu huku akiwaonya wenye lengo la kufanya vurugu na kusema hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Rais Kikwete ametoa kauli hiyo katika wakati wa hitimisho la kampeni za Chama cha Mapinduzi visiwani Zanzibar eneo la Chakechake, Pemba katika uwanja wa bombani ya kale na kusema wananchi wajitokeze kwa wingi Oktoba 25 kupiga kura.

Aidha Rais Kikwete amewahakikishia usalama wananchi na kusema kuwa utalindwa na kuangaliwa kwa umakini kwa kuwa tayari jeshi la polisi limejipanga vya kutosha kuhakikisha uchaguzi unaisha kwa amani na utulivu.

Kwa upande wake mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi Visiwani humo Dkt. Ali Mohammed Shein amesisitiza kuwepo kwa uchaguzi wa amani visiwani humo na kuongeza kuwa yale yote aliyoahidi basi yatatekelezwa katika kipindi chake.

Naye mgombea mwenza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupita chama hicho Bi. Samia Suluhu amewataka vijana wasidanganyike na maneno ya wanasiasa ambayo yatawafanya kuvuruga amani.