Jokate aipokea Namthamini, wanafunzi wanufaika

Jumamosi , 14th Dec , 2019

Zoezi la ugawaji wa pedi kwa wanafunzi wa kike katika shule mbalimbali nchini kupitia kampeni ya Namthamini, limeendelea katika mkoa wa Pwani, ambapo shule mbili za wilaya ya Kisarawe zimenufaika na kampeni hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo (katikati) akipokea taulo za kike. Kushoto ni Mtangazaji TBway na kulia ni Deogratius Kithama.

Shule hizo ni Kibuta Sekondari ambayo ilipatiwa jumla ya pakiti 804 kwaajili ya wanafunzi 80 na watatumia kwa zaidi ya mwaka mmoja, hivyo kuwa na uhakika wa kutokosa masomo kwa changamoto ya kukosa pedi wakati wa hedhi.

Shule ya pili ni Maneromango Sekondari ambayo ilipatiwa jumla ya pakiti 1086 kwaajili ya 108, ambayo pia watakuwa na uhakika wa kuwa na taulo za kike kwa mwaka mzima.

Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo, alishiriki kupokea taulo hizo katika shule zote akiwa ameambatana na timu ya East Africa Television na East Africa Radio.

Baada ya kupokea taulo hizo Mh Jokate aliwasihi wanafunzi kuona kama ni nafasi ya kujituma kwenye masomo ili kuwapa motisha watu waliochangia kuweza kuwasaidia tena.

'East Africa TV na East Africa Radio ni kampuni kubwa sana, wameacha kazi zao kwaajili ya kuja kuwathamini nyie, kwahiyo mnatakiwa muwalipe kwa kujituma na kufanya vizuri kwenye masomo yenu ili warudi tena', alisema Jokate.

Aidha Jokate aliishukuru East Africa Television na East Africa Radio kwa kuweka wazi kuwa zimemsaidia katika kampeni yake ya Tokomeza Zero Kisarawe kwa kutoa pedi hivyo kupunguza tatizo la utoro kwa wanafunzi wa kike wanapokuwa katika hedhi.