JPM ashangaa waliozaliwa porini na wasile nyama

Alhamisi , 10th Oct , 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ameiagiza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa mkoani Katavi kuhakikisha inakuwa na duka litakalokuwa linauza nyama za wanyamapori wanaopatikana katika Mbuga ya mkoa huo japo mara moja kwa wiki.

Rais Magufuli

Rais Magufuli ameyabinisha hayo leo Oktoba 10, 2019, wakati wa uzinduzi wa Barabara inayotoka Mpanda hadi Mkoani Tabora katika ziara yake ya siku tatu mkoani Katavi, ambapo amesema kuwa kwa kufanya hivyo hakutaweza kuwamaliza wanyamapori waliopo katika hifadhi.

''Lakini pia nimeagiza fungueni duka la nyama ya porini, sio kila siku watu wakitamani hata kanyama ka Swala kuingia kule ni kazi, wekeni utaratibu wa kuuza hata mara moja kwa wiki, haiwezekani mtu wa Katavi, umezaliwa porini hadi ufe meno yako hayajawahi kuonja nyama ya porini hata ya Ngiri, hawa wanyama hawawezi wakaisha, ndiyo faida ya kuwa na wanyama karibu'', amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amewaomba wakazi wanaozunguka Hifadhi ya Taifa ya Katavi, wasiende kuvamia eneo hilo na kuwaua Wanyamapori na badala yake wasubiri utaratibu wa uuzaji wa nyama utakaowekwa na TANAPA.