Jumatatu , 3rd Dec , 2018

Kiongozi wa kanisa katoli duniani, Papa Francis, ametoa tamko kuhusu viongozi wa kanisa hilo kujihusisha na ushoga, na kusema kwamba kanisa haliruhusu vitendo hivyo.

Akihojiwa na Mmishenari mmoja kutoka nchini Uhispania aliyejulikana kwa jina la Fernando Prado kuhusu wito wa kidini na vitendo vya ushoga kwa ajili ya kitabu anachoandika kinachoitwa 'Nguvu ya Utumishi' , Papa Francis amesema kwamba kanisa katoloki halitaruhusu mtu yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo, kuingia kwenye utawa.

Papa amesema mahusiano ya jinsia moja ni jambo la "fasheni" ambalo sasa limeshika hatamu duniani, na kutaka makasisi kutii viapo vyao vya utawa (kutojihusisha na mapenzi).

“Hili suala la mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja ni kubwa sana, kwa sababu hiyo, Kanisa linawataka watu wenye tabia hizo (wapenzi wa jinsia moja) wasikubaliwe katika maisha ya ukasisi”, amesema Papa Francis.

"Katika jamii zetu, sasa inaonekana kuwa suala hili la mapenzi ya jinsia moja limekuwa fasheni. Mawazo kama hayo sasa yanaanza kupata ushawishi ndani ya kanisa, suala hili katu halina nafasi katika maisha ya watawa wetu." aliongeza Papa Francis.

Pamoja na hayo Papa Francis amesema kwamba iwapo mtu amnayejihusisha na mapenzi ya jinsia moja kutaka kuwa karibu na Mungu, yeye hawezi kumuhukumu.

"Kama mtu ni shoga na anataka ukaribu na Mungu na ana nia njema, mimi ni nani wa kuhukumu?," amesema Papa Francis.